Je wewe ni mwandishi wa habari unayechipukia au mwandamizi, mwenye shauku ya kujikita katika kuandika habari za afya ya uzazi, biashara na uchumi au nishati na madini? Unatamani kusafiri nchini katika maeneo ya pembezoni au vijijini ili kuandika mambo yaliyofichika na hatimaye kuibua mjadala na hatua kuchukuliwa?
Unataka kunoa ujuzi wako wa kiuandishi na ubunifu chini ya usimamizi wa waandishi na wataalamu magwiji wa nchini na kimataifa; ambao watabadili mtazamo wako katika uchambuzi na uelewa wa mambo? Basi Mpango huu wa ‘Fellowship’ ni wako!
Mfuko wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF) unalenga kukuza uhuru na ubora katika vyombo vya habari, msisitizo ukiwa katika habari zinazogusa jamii na za uchunguzi. Mfuko unaamini vyombo huru vya habari ndio kiini cha jamii huru na ya kidemokrasia.
Mfuko sasa unapokea maombi kutoka kwa waandishi wa habari za magazeti kwa Mpango wa ‘Fellowship’ wa 2012. Mwisho wa kupokea maombi ni Juni 15, 2012. Mpango huu wa miezi sita uko wazi kwa waandishi Watanzania 10.
Sifa za waombaji:
- Utashi wa kufanya kazi ya uandishi wa habari nchini Tanzania
- Awe ameandika habari/makala katika nyanja tofauti na angependa kujikita zaidi katika kuandika habari za afya ya uzazi, biashara au uchimbaji madini (mafuta na gesi vikiwemo).
- Awe tayari kusafiri nchini katika maeneo ya pembezoni au vijijini kwa kipindi cha wiki sita wakati wa Mpango wa ‘Fellowship’.
- Ufahamu wa Kiingereza na Kiswahili
- Ujuzi katika mitandao ya kijamii ni sifa ya ziada
Maombi yaambatanishwe na:
Maelezo kuhusu elimu ya muombaji (CV)
Maneno 300 – 500 kuhusu ushawishi wako wa kuomba na maelezo zaidi kuhusu uzoefu wako katika uandishi wa habari, malengo na mipango yako katika tasnia ya habari; nini kilichokuhamasisha kuomba mpango huu wa ‘Fellowship’ 2012.
Maneno 300 – 500 kuhusu moja ya wazo la habari unaloomba, kama ni katika Afya ya Uzazi, Biashara, uchumi au nishati na Madini. Hata hivyo, ombi lingine lolote nje ya maeneo yaliyotajwa linaweza kutazamwa kulingana na umuhimu wake na jinsi muombaji atakavyolijengea hoja.
Barua mbili za mapendekezo; moja kutoka kwa mtu anayejua kazi zako – anayeweza kuzungumzia uwezo wako kiuandishi na nyingine kutoka kwa mhariri wako.
Barua ya ruhusa ya kushiriki kwenye mpango kutoka kwa mwajiri wako na inayothibitisha kwamba kazi zako zitachapishwa au kuwekwa kwenye mitandao ya kijamii.
Mfano wa kazi zako tatu zilizowahi kuchapishwa.
ANGALIZO: Mpango huu wa ‘Fellowship’ haukusudii kutoa mafunzo ya awali kwa waandishi wa habari. Hivyo basi, washiriki wanatarajiwa kuwa waandishi wenye ujuzi katika fani ya uandishi wa habari.
Washiriki watapata fursa ya kusafiri sehemu mbali mbali nchini kwa lengo la kuandika habari zinazohusiana na nyanja walizochagua na kwa wao kuwa wa kwanza kuandika habari hizo kwa kina. Aidha, watanufaika na mfululizo wa semina na warsha kutoka kwa wataalamu katika masuala ya Afya ya Uzazi, Biashara, uchumi na Uchimbaji Madini. Semina hizi ni sehemu ya mpango wa ‘fellowship’ wa kupanua mtazamo wa washiriki katika mambo mbali mbali ya kijamii.
Mpango huu utaanza Julai, 2012 hadi Desemba, 2012. Washiriki watapewa fedha za kujikimu pamoja na kugharamiwa usafiri na vitendea kazi.
Tuma maombi yako:
Tanzania Media Fund
2012 Fellowship Programme,
S.L.P 38266
Dares Salaam
Barua pepe: fellowship@tmf.or.tz
Kwa maulizo zaidi kuhusu mpango huu, sifa zinazohitajika na uombaji wasiliana kupitia:- fellowship@tmf.or.tz au kwa simu namba 0713 757545 wakati wa kazi tu.
No comments: